Followers

Thursday, May 9, 2013

KISAA CHA BILAL....MUADHINI WA MWANZO KATIKA UISLAMU.
Bilaal Bin Rabaah (Radhiya Allaahu 'Anhu)

‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa kila linapotajwa jina la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akisema;

"Bwana wetu aliyemkomboa Bwana wetu". Akimkusudia Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ‘anhu). Wanasema wanavyuoni kuwa; Unapomsikia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akimwita mtu 'Bwana wetu', basi tambua ya kuwa huyo ni mtu adhimu.

Imeandikwa katika Siyar al-A’alaam an-Nubalaa kuwa Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye asili yake ni Mhabeshi (mu-Ethiopia), alikuwa mweusi sana, mwembamba, mrefu na mwenye nywele ndefu.

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtumwa wa kabila la Bani Jumhi, na maisha yake yalikuwa kama mtumwa yeyote wa kawaida pale Makkah, hakuwa na uwezo wala uhuru wowote isipokuwa kuwatumikia mabwana zake watu wa kabila la Al-Jumhi. Baadaye alimilikiwa na Umayyah bin Khalaf peke yake ambaye pia anatokana na kabila hilo la Al-Jumhiy, na mama yake Bilaal na jina lake lilikuwa Hamaamah, naye pia alikuwa mtumwa wa kabila hilo la Al-Jumhi.
Mara baada ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuanza kuwalingania watu katika dini ya Kiislam kwa jahari, Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa anasikia habari za dini hii mpya na habari za Mtume huyu mpya (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na habari hizo zilikuwa zikimfurahisha sana kila anapozisikia hasa kutoka kwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa kila anapopata fursa akimwendea Bilaal na watu wengine pia na kuwahadithia juu ya dini hii.
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasilimu mikononi mwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akifanya kazi kubwa sana tokea siku ya mwanzo katika kuwalingania watu katika dini hii tukufu.
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiwalingania watu waliokuwa huru na akafanikiwa kuwasilimisha watu watukufu wakiwemo watano katika wale kumi waliobashiriwa Pepo nao ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Az-Zubayr bin ‘Awaam, ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf, Sa’ad bin Abi Waqaas na Twalha bin ‘UbayduLlaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wengi wengineo, na alikuwa pia akiwalingania watu wasiokuwa huru kama vile Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa rafiki yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) tokea hata kabla ya Uislam, na wengineo pia.
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifuatana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuzitamka shahada mbili mbele yake, na kwa ajili hiyo akawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini hii tukufu.


Ahadun Ahad

Uislam ulipoanza kuenea katika mji wa Makkah, na baadhi ya Ma-Quraysh kutambua kuwa watumwa wao walikuwa wakiingia katika dini hii mpya kwa siri tena kwa wingi, wakaanza kuwatesa kwa kuwaonjesha kila aina ya adhabu.
Miongoni mwa Waislam wa mwanzo waliokuwa watumwa na wakapata adhabu kubwa kutoka kwa washirikina wa Makkah, ni Sumayyah, mama yake ‘Ammaar aliyekuwa mke wa Yaasir (Radhiya Llaahu ‘anhum) waliokuwa na asili ya Ki-Yemen.
Walikuwa wakiadhibishwa sana, na kila Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anapopita nje ya nyumba yao alikuwa akiwaambia;

"Kuweni na subira enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwani hakika waadi wenu ni Pepo".

Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alifariki akiwa anateswa na akapata bahati ya kuwa Shahid wa mwanzo katika dini ya Kiislam.
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye alipata sehemu kubwa ya adhabu, kwani bwana wake Umayyah bin Khalaf aliyekuwa mtu khabithi sana, alikuwa akimtoa nje wakati wa jua kali linalounguza mwili na kumvua nguo zake kisha anamlaza juu ya mchanga wa jangwani unaounguza na kumwekea jiwe kubwa sana juu ya kifua chake huku akimwambia;

"Utabaki hivyo hivyo mpaka ufe isipokuwa kama utamkanusha Muhammad na kumtukana kisha urudi tena kuiabudu miungu yako Lata na Uzza".

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akimjibu kwa kusema;

"Ahadun Ahad".(Mmoja tu, mmoja tu)

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwahi kuulizwa;

"Kwa nini ulikuwa ukiendelea kusema hivyo "Ahadun Ahad".(Mmoja tu, mmoja tu), na hali unajua kuwa maneno hayo yanawaghadhibisha na kwa ajili hiyo wao wataendelea kukuadhibu?"

Akajibu;

"WaLlaahi kama ningekuwa nalijuwa neno jingine linaloweza kuwakasirisha zaidi kuliko hilo, basi ningelilitamka".
Hakika neno; "Ahadun ahad", lilikuwa likimkera sana Umayyah na kila anapolisikia alikuwa ghadhabu zinampanda na akawa anampiga Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama mwendawazimu.

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa anaendelea kuadhibishwa na yeye alikuwa akiendelea kustahamili huku akiendelea kulitamka neno lake hilo 'Ahadun ahad', mpaka Umayyah mwenyewe akashindwa, kwani kila siku baada ya kumtesa wakati wa mchana, alikuwa akimfunga kamba shingoni na kuwakabidhi watoto wadogo na wendawazimu waliokuwa wakimburura Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kuzunguka naye mjini Makkah, huku wakimzomea na kumpiga, na yeye alikuwa akiendelea kusema'

"Ahadun ahad" (Mmoja peke yake mmoja peke yake).

Na Amchae Mungu

Siku moja Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akipita akamuona Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika hali ile, akamwambia Umayyah;
"Humuogopi Mungu wewe, unamtesa namna hii maskini huyu, mpaka lini utaendelea hivi?'

Umayyah akamwambia;

"Wewe ndiye uliyemharibu huyu, kwa hivyo sasa muokoe wewe kama unaweza".
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamnunua kwa wakia tano na akamuacha huru kwa ajili ya kutaka Radhi za Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa keshawanunua watumwa sita na kuwaacha huru, na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa wa saba.
Bilaal akaepukana na adhabu, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) bila shaka akapata ujira mkubwa kutoka kwa Mola wake (Subhanahu wa Ta’ala).

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliendelea na kazi hiyo ya kuwanunua watumwa na kuwaacha huru, na Maulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa Mwenyezi Mungu Alimsifia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika Aya ya 17 katika Suratul Layl pale Aliposema;

“Na amchaye (Mwenyezi Mungu) ataepushwa nao (Moto).
Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.

Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.

Isipokuwa (anafanya haya) kwa kutaka radhi ya Mola wake Mtukufu.
Basi atapata la kumridhisha.”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaondoka hapo pamoja na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kwenda mpaka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na alipokuwa akiondoka naye, Umayyah akamwambia;
"Ondoka naye hapa, Naapa kwa Laata na Uzza, kuwa ungekataa kumnunua kwa wakia tano, basi hata kwa wakia moja tu ningekuuzia".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;

"WALLAHI, LAU KAMA UNGETAKA NIMNUNUE KWA WAKIA MIA, BASI NINGEKUPA".

Muadhini Wa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Wa Mwanzo

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alifurahi kupita kiasi alipomuona Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa huru, na akawabashiria Waislam juu yake na akamfanya baadaye kuwa ni Muadhini wake wa mwanzo katika Uislam, kwani Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na sauti nzuri sana na Mwenyezi Mungu Akaijaalia sauti hiyo iwe yenye kuleta taathira ndani ya nyoyo za kila mwenye kuisikia.
Mji wa Madiynah ulikuwa ukitulia pale anapoadhini Bilaal, na watu walikuwa wakikimbilia Msikitini mara baada ya kuisikia sauti yake (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pia alikuwa akimpenda sana Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) na akistarehe sana kila anapoisikia sauti yake, na hasa anapoadhini, na alikuwa akiwatanguliza Bilaal na watu masikini miongoni mwa Waislam kabla ya matajiri na alikuwa akikaa nao muda mrefu zaidi na alikuwa akiwakirimu.
Siku ile Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipoingia na majeshi yake kuuteka mji wa Makkah, na baada ya kusafishwa msikiti wa Makkah kutokana na masanamu yaliyokuwa yamejaa humo, aliingia Msikitini na kuufunga mlango nyuma yake akiwa yeye na Bilaal na ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) peke yao ndani ya Msikiti na katika riwaya nyingine aliingia pia na ‘Uthmaan bin Twalha (Radhiya Allaahu ‘anhu), na kuwaacha watu wa kabila lake na watu wa nyumba yake pamoja na Maswahaba wakubwa wakubwa kama vile Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhum) nje ya Msikiti.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamtaka Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) apande juu ya Al-Ka’abah na kuadhini, na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akafanya kama alivyoamrishwa, na jambo hili liliwakasirisha sana baadhi ya Ma-Quraysh, akasema Itab bin Usayd;
"Nashukukru baba yangu hajaishi mpaka akaweza kuyaona haya! Hivyo Muhammad hajapata mwengine wa kutuadhinia isipokuwa kunguru huyu mweusi?"
Bilaal na ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) wote walikuwa watumwa kabla ya Uislam.
Na katika hadithi, siku moja Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuuliza Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu);
"Nielezee juu ya ‘amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako vikiwa mbele yangu Peponi?"

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu;

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu sijafanya ‘amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikitawadha huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali”.
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia;

“Hilo ndilo lililokufikisha”.
Al-Bukhaariy


Baadhi Ya Sifa Zake

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuwa akimiliki sauti nzuri tu, bali alikuwa pia shujaa na alishiriki katika vita vyote walivyopigana Waislam, vile alivyoshiriki Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ndani yake na pia vile asivyoshiriki, na alikuwa mpiganaji mzuri sana. Alishiriki katika vita vya Badr na kupigana kwa ushujaa mkubwa, na yeye ndiye aliyemuua Umayyah bin Khalaf baada ya kutekwa na Waislam katika vita hivyo.
Ingawaje daraja yake ilikuwa mbele ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na mbele ya Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhu), lakini Bilaal hakuwa mtu mwenye kujiona wala kujivuna wala mwenye kutakabari, bali alikuwa mnyenyekevu kwa Waislam wenzake, huku akiichunga nafsi yake, jambo lililomfanya aheshimiwe zaidi na Maswahaba wenzake (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Kuposa Kwake

Katika kitabu cha Siyar al-A’alaam an-Nubalaa cha Imaam Adh-Dhahabiy na katika Al-Bidaayah wan-Nihaayah cha Ibn Kathiyr imeandikwa kuwa; Siku ile alipokwenda yeye na ndugu yake kuposa katika nyumba moja ya watu wa kabila la Ki-Yemen, aliwaambia;
"Mimi ni Bilaal na huyu ni ndugu yangu Abshan, sisi ni watu wa Uhabeshi, tulikuwa tumepotoka na Mwenyezi Mungu Akatuongoza, na tulikuwa watumwa na Mwenyezi Mungu Akatukomboa. Kama mtakubali kutuozesha watoto wenu, 'AlhamduliLlaah' tunamshukuru Mwenyezi Mungu, na kama mtatukatalia basi 'Allaahu Akbar' Mungu ni Mkubwa".
Bilaal na ndugu yake waliowa katika nyumba hiyo.

Siku Aliyofariki Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

Maisha yake yote Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), tena karibu naye. Kila siku akimuadhinia huku Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akifurahishwa na sauti yake na yeye kwa upande wake alibahatika kuweza kuyatia nuru macho yake kila siku kwa kumuona kipenzi cha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) asubuhi na jioni, mchana na usiku, mpaka siku ile Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipoisalimisha roho yake kwa Mola wake.
Siku ile, Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliingia chumbani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa ajili ya kumtizama kipenzi chake kwa mara ya mwisho, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa amefunikwa na kulazwa juu ya tandiko lake, na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa anamtizama huku machozi yakimlenga. Aliposhindwa kuimiliki nafsi yake akaanza kulia kwa kwikwi.na baada ya muda akatulia, kisha akasogea mbele yake na kumswalia. Baada ya kumswalia akatoka chumbani huku machozi yakiwa yanaendela kumiminika.
Usiku uliofuata Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kupata usingizi hata kidogo kutokana na huzuni iliyomjaa moyoni mwake, na hasa kila anapokumbuka kuwa hatoweza kumuona tena Swahibu yake kama alivyokuwa akimuona kila siku mbele ya macho yake. Akawa katika hali hiyo usiku kucha mpaka ulipokaribia wakati wa Swalah ya Alfajiri alipotoka na kuelekea Msikitini kama kawaida yake kwa ajili ya kuadhini, na ulipoingia wakati wa adhana akaanza kuadhini;

"Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu Akbar Allaahu Akbar. Ash-hadu an laa ilaaha illa Llaah, Ash-hadu an laa ilaaha illa Llaah…" Alipotaka kutamka;
"Ash-hadu anna Muhammadan Rasuulu Llaah", Akashindwa, - pumzi zilimkaba, sauti ikashindwa kutoka, na aliposhindwa kuimiliki nafsi yake, machozi yakaanza kummiminika, na watu waliposikia kukatika kwa adhana na kilio cha Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) wote waliokuwepo Msikitini nao pia wakaanza kulia. Na baada ya kuweza kuimiliki nafsi yake, Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaikamilisha adhana kwa sauti ndogo na hakuweza kuinyanyua sauti yake.

Baada ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuzikwa, Bilaal akaondoka na kujitenga mbali kidogo na watu huku akilia kwa huzuni. Ulipoingia wakati wa Swalah, watu wakawa wanamsubiri Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) awastareheshe kwa kuwaadhinia kwa sauti yake nzuri. Lakini Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuadhini. Watu wakamkumbusha kwa kumwambia;

"Wakati wa adhana ushaingia ewe Bilaal".

Akasema huku machozi yakimlenga;

"Sitoadhini tena baada ya leo, bora aadhini mwengine badala yangu."

Sitoadhini Tena Baada Ya Kufa Kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

Wakati wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa Khalifa wa Waislam, alimtaka Bilaal aadhini akamwambia;
"Adhini".
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikataa, akamwambia;

"Ikiwa ulinikomboa kwa ajili ya nafsi yako basi nikamate, ama ikiwa kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, basi niache na Mungu wangu."
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;
"Nilikukomboa kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu Peke Yake".

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu kwa huzuni;

"Basi mimi sitoadhini tena baada ya kufa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)".

Baada ya kufariki Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akataka kwenda kupigana Jihaad, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimkatalia, akamwambia;
"Nakuomba kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ewe Bilaal, kwa hisani yako, umri wangu ushakuwa mkubwa na siha yangu ishadhoofika na ajali yangu ishakaribia, tafadhali baki hapa pamoja na mimi".

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akakubali kuwa pamoja naye mpaka Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipofariki dunia.
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Anakwenda Kupigana Jihaad
Alipotawala ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), naye pia alimtaka Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aadhini, naye akamkatalia pia ombi lake hilo, kisha ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamuuliza;

"Yupi unaona nimpe kazi ya kuadhini?"
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Sa’ad, kwani yeye aliwahi kuadhini wakati wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)".

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwendea ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumuomba amruhusu kwenda kupigana Jihaad.
‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;
"Ewe Bilaal, hutaki kubaki pamoja nami kama ulivyokuwa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kisha pamoja na Abu Bakr?"
Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Natamani kwenda kupigana Jihaad ewe Amiri wa Waislam, na naona kuwa Jihaad ni miongoni mwa ‘amali bora kupita zote".‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia;

"Fanya kama unavyotaka ewe Bilaal."

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasafiri kuelekea nchi ya Shaam na kujiunga na jeshi lililokuwa likiongozwa na Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Jarraah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Bilaal (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Anaadhini Tena

Alipoitembelea nchi ya Shaam wakati wa Ukhalifa wake, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alionana tena na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Waislam wakamuomba ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) awaombee kwa Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) ili awaadhinie angalau mara moja tu ili wapate kuisikia sauti yake ‘adhimu aliyokuwa akiinyanyua kila siku mara tano wakati wa uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Ulipoingia wakati wa Swalah, ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamuomba Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aadhini na Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akalikubali ombi lake, akapanda juu ya mlmbari na kuanza kuadhini. Nyoyo za watu zilikuwa zikipiga kwa nguvu huku wakiisikiliza sauti ya Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiadhini kwa mara ya mwanzo tokea alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imeandikwa katika kitabu cha Siyar A’alaam an-Nubalaa kuwa;

"Watu hawakupata kulia kama siku hiyo kwa ajili ya kukumbuka uhai wa Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)".

Kifo Chake (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Haya kwa ufupi ni maisha ya Swahaba huyu mtukufu (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyejitolea nafsi yake kwa ajili ya kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu.
Alifariki katika mji wa Damascus mwaka wa ishirini baada ya Hijrah ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa ana umri uliopindukia miaka sitini kwa maradhi ya tauni yaliyowaua watu wengi sana katika nchi ya Shaam.
Inasemekana kuwa roho yake ilipokuwa ikimtoka, mkewe alikuwa akimwambia;
"Huzuni iliyoje, huzuni iliyoje."

Lakini Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiyafumbua macho yake akasema;
"Bali furaha iliyoje, kesho nitaonana na wapenzi, Muhammad na Maswahaba."

No comments:

Post a Comment

10 Ways of Protection from Shaytan:

Imam Ibn ul Qayyim

Seeking refuge with Allah from Shaytan. Allah the Most High said, “And if there comes to you from Satan an evil suggestion, then seek refuge in Allah. Indeed, He is the Hearing, the Knowing.” [41:36]

Recitation of the two soorahs al-Falaq and an-Nas, as they have wondrous effect in seeking refuge with Allah from evil, weakening Shaytan and protection from him. This is why the Messenger, sallallahu `alayhi wa sallam, said: “No person seeks refuge with anything like the Mu`awwidhatayn (soorahs al-Falaq and an-Nas)”. [an-Nasaa’i, 5337]

Recitation of Ayat al-Kursi (2:255).

Recitation of soorah al-Baqarah. The Messenger, sallallahu `alayhi wa sallam, said, “The house in which al-Baqarah is recited is not approached by Shaytan.” [Muslim]

The final part of al-Baqarah. The Messenger, sallallahu `alayhi wa sallam, said, “Whoever recites the two last verses of al-Baqarah at night they will suffice him.” [Muslim]

Recitation of the beginning of soorah Mu’min (Ghafir), until His saying, “wa ilayhi-l-maseer” (to Him is the destination). (i.e. “Ha. Meem. The revelation of the Book is from Allah, the Exalted in Might, the Knowing, the forgiver of sin, acceptor of repentance, severe in punishment, owner of abundance. There is no deity except Him; to Him is the destination.” [40:1-2])

Saying “la ilaha ill Allah wahdahu la sharika lah, lahul mulku wa lahul hamdu wa huwa `ala kulli shay’in qadir” (there is nothing worthy of worship except Allah, He has no partner, His is the Dominion and Praise, and He is able to do all things) a hundred times.

The most beneficial form of protection from Shaytan: abundance of remembrance of Allah, the Exalted.

احمد محب الدين الأخبار جديد/احب الله ورسوله

حبّ الرسول صلّى الله عليه وسلّم

قال عليه والصلاة والسلام <<من أحبّ سنّتي فقد أحبّني ومن أحبني كان معي في الجنة>>وقال تعالى<<قل إن كنتم تحبّون الله فاتبعوني يحبب كم الله و يغفر ذنوبكم>>

Popular Posts