|
Gedeon Kyungu Mutanga huwaambia vijana kuwa wanapigania maisha mazuri |
Baada ya muasi mkubwa na anayesifika sana kutoroka
jela Katanga, mkoa huo wenye madini chungu nzima uliokuwa thabiti
umekuwa ukivurugwa kwa mwaka mmoja uliopita na kundi linalotaka eneo
hilo kujitawala.
Mkoani Katanga, ni kawaida kuwasikia watu
wakilalamika kuwa hawajanufaika sana kutokana na madini yaliyo kwenye
mkoa huo, mfano Shaba nyekundu na Cobalti kwa hivyo sio jambo la
kushangaza kuwa vijana wengi waliitikia wito wa eneo hilo kujitenga.
Chini ya wiki moja baada ya uhuru wa
Congo mwezi Juni mwaka 1960, ulitangaza kuwa unajitenga na hivyo kuzua
mgogoro uliochochewa na uhasama uliotokana na vita baridi.
Kiongozi wa wale waliotaka kujitenga Moise
Tshombe ambaye pia alikuwa mfanyabiashara , aliungwa mkono na Ubelgiji,
Marekani na Uingereza zote zenye maslahi ya uchimbaji madini.
Baada ya miezi minne, waziri mkuu wakati huo
Patrice Lumumba alipinduliwa na baadaye akauawa huku Tshombe akirejeshwa
kwenye jeshi kutokana na shinikizo kutoka kwa Umoja wa Mataifa na
Katanga kufanywa kuwa sehemu ya DRC mwaka 1963.
Siasa za vita baridi huenda sio hoja kwa mkoa huo wenye kuzungumza Kiswahili, na ambao ni wenye ukubwa sawa na Ufaransa.
Zamani mbinu iliyokuwa inatumiwa sio ya sasa.
Wapiganaji wa vuguvugu la Mai Mai hawatumii mbinu zitakazowafurahisha
wenyeji wa mkoa huo.
''Walimfungia mamangu kwenye mti na kumdunga kwa
mshale,'' alisema Antoinette mwenye umri wa miaka 18 akikumbuka
mashambulizi yaliyofanywa katika kijiji chake cha Montofita ambapo
baadhi ya nyumba ziliteketezwa na mamake kutekwa nyara.
"walikata matiti yake na niliona kila kitu kwa
macho yangu. Kisha kila mwanamume akanibaka. Majirani zangu walizikwa
wakiwa hai,'' alisema Antoinette.
|
Kijiji cha Pueto ni makao kwa maelfu ya wakimbizi waliotoroka Katanga |
Antoinette amepata hifadhi katika kijiji cha
Pweto katika eneo la mpakani na Zambia ambako zaidi ya watu laki sitini
pia wamepata hifadhi.
Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNCR,
linakadiria kuwa zaidi ya 1,700 walioachwa bila makao ni wanawake na
wengi walibakwa kabla ya kutoroka.
Takriban watu laki nne waliachwa bila makao na sasa wamepata hifadhi katika kambi za wakimbizi.
"labda ikiwa wenyeji wa Katanga wangewaunga
mkono waasi hao wa Katanga, lakini waasi hawakutupa nafasi, walianza
kutuua na kuchoma nyumba zetu. Sio kama watu wanaopigania ukombozi,''
asema Priscille,mkimbizi anayeishi katika kijiji cha Pweto.
Kuna makundi mengi ya wapiganaji wa Mai Mai, neno hilo likitumiwa na makundi yaliyojihami mkoani humo.
Usajili vijijini
Kata Katanga, neno la kiswahili linalomaanisha
Katanga ijitawale, lilibuniwa baada ya Gedeon Kyungu Mutanga kutoroka
jela mwezi Septemba mwaka 2011.
Kabla ya kufungwa jela mwaka 2006, alikuwa
kiongozi wa kundi la waasi ambalo lilisaidia jeshi la Congo kupigana na
waasi kutoka Rwanda miaka ya tisini.
Baada ya kumalizika kwa mgogoro huo,alidaiwa kuendelea kupokea msaada wa mtu aliyekuwa jeshini.
Hata hivyo baada ya kutoroka alisemekana bado alikuwa anapokea msaada wa kifedha kutoka kwa mtu aliyekuwa anaishi ughaibuni.
Mwanamume mmoja aliyetoroka kundi hilo la waasi
akiwa na wake wawili pamoja na watoto wanane, aliambia BBC ambavyo
kundi hilo huwasajili wapiganaji kwani huwashawishi vijana kujiunga na
waasi hao wakipigania maslahi yao na kuwa hawakuwahi kumuona kwa macho
yao kwani alikuwa akijificha chumbani wakati akiongea nao.
Katanga ina utajiri mkubwa sana , lakini wanachi wanahisi kuwa hawafaidi vyovyote.
Madini ya Cobalt yako kwa wingi zaidi katika
mkoa huu kuliko sehemu yoyote nyingine duniani na mkoa huu ni wa pili
kwa ukubwa katika uzalishaji wa Shaba nyekundu.
Wakati maelfu ya watu wakitembea siku hizi
kwenye barabara zenye vumbi, kutoroka waasi hao, barabara zengine
hutumiwa kusafirisha madini yenye thamani ya mamilioni ya dola nje ya
nchi.
|
Ni familia chahe sana ambazo zimepewa mahema na umoja wa mataifa wengi hulazimika kujijengea |
Malori mengi yenye madini ya Cobalt na Shaba nyekundu, huonekana yakiwa yamepanga foleni kuingia Zambia
Kulingana na sheria ya DRC serikali inapaswa
kuupatia mkoa huo asilimia 40 ya kodi zinazotozwa makampuni ya uchimbaji
kwa mkoa wa Katanga lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu
yanasema kuwa pesa hizo hazijafaidi chochote.
Lucien,ni mwalimu wa shule kutoka Kabisa ingawa
sasa anaishi kijiji cha Pweto, anasema kuwa mamia ya vijana wamejiunga
na wapiganaji wanaopigania uhuru wa Katanga kutoka kwa kijiji anakoishi.
"Nililengwa kwa sababu nina elimu , mimi
huwambia watu ukweli wa mambo na kwa hivyo builiwashawqishi vijana
kutojiunga na waasi hao, '' aliambia BBC
''Niliwaambia kuwa mwishowe wangetaabika tu.''
Kulingana na maafisa wakuu katika kijiji cha
Pweto, mamia ya wapiganaji wa Mai Mai wameondoka jeshini tangu mwanzoni
mwa mwaka huu, wakiwa wamechoka na kuishiwa na matumaini.
"Hatutawahi kupata uhuru. Leo tuko maskini zaidi
kuliko miaka ya nyuma, wengi wetu wamefariki,'' alisema mpiganaji mmoja
aliyekuwa katika vuguvugu hilo.
Mnamo mwezi Machi karibu wapiganaji 200 wa Kata
Katanga wakiwa wamejihami na kubeba bendera za kutaka ukombozi wa
Katanga waliingia Lubumbashi.
Walipeperusha bendera yao kabla ya kujisalimisha
kwa UN baada ya makabiliano makali ambapo wapiganaji 23 waliuawa.
Tangu hapo wapiganaji hao wametishia kwa mara nyingine kuvamia mji huo.
Je unaweza kuwalaumu waasi kwa kuchukua silaha
wakidai maslahi yako ambayo ni haki yao huku wakitaka uhuru wao? Baadhi
wanasema wanaona uhuru wa Katanga ukiwa kitu kizuri lakini inategemea
wataupata kwa njia gani.
Waziri mkuu wa DRC Matata Ponyo, anasema kuwa
hapa hakuna uasi akiongeza kuwa watu wana haki ya kudai haki zao kwa
njia ya kidemokrasia na kuwa serikali itajitahidi kukabiliana na makundi
kama hayo.